Friday, April 6, 2012

TABORA GIRLS' SECONDARY SCHOOL


current photo of infront of taboragirls

Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora  iliyoanzishwa mwaka 1928 kama shule ya msingi kwa wakati huo wa ukoloni, ilijulikana kwa jina la African Girls School. Shule hiyo yenye ukubwa wa hekta zaidi ya 97, ilianzishwa na wakoloni wa Kiingereza kwa madhumuni ya kutoa elimu kwa watoto wa kike wa machifu.

Mwaka 1957, shule ilipewa hadhi ya kuwa sekondari ya wasichana ambapo mwaka 1972 ilianza kusajili wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi (albino) na wasioona.

Kaulimbiu ya shule ni strive to excel yaani kazana ufanikiwe, huu ni ukweli unaobainishwa na uwepo wa wanataaluma waliobobea katika fani ya sheria, udaktari, uhandisi, ualimu na hata katika siasa waliosoma katika shule hiyo.

Miongoni mwa viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Mke wa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa sawa kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa, aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika na Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongella.

Wengine ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Margareth Sitta na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Buriani.

Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Celina Kombani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT- Taifa) Anna Abdallah, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk. Joyce Ndalichako.

Wamo pia Jaji mstaafu Julie Manning, Jaji wa Mahakama Kuu, Eusebia Munuo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani (UN Habitat), Profesa Anna Tibaijuka. Nidhamu ya shule hiyo ni jambo ambalo linawasaidia wanafunzi wasomao shuleni hapo kuwafungulia milango ya mafanikio katika maisha yao.

Monday, April 2, 2012